Home > Press Release> Umoja wa wanafunzi wanaosoma nchini Kenya wajitokeza kuchangia katika kampeni ya ujenzi wa hosteli za wasichana

Umoja wa wanafunzi wanaosoma nchini Kenya wajitokeza kuchangia katika kampeni ya ujenzi wa hosteli za wasichana

March 17, 2014

 Umoja wa wanafunzi wanaosoma katika chuo cha  United States International University (USIU) nchini Kenya umewasilisha mchango wao wenye thamani ya shilingi 300,000/= katika kuchangia kampeni ya ujenzi wa hosteli za wasichana inayoendeshwa  na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Akiwasilisha mchango huo kwa niaba ya wanafunzi hao, Mwenyekiti wa umoja huo Ester Lugoe amesema kwamba, lengo la umoja huo ni kutoa shilingi laki tano lakini kwa kuanza wamekabidhi jumla ya shilingi laki tatu na kuahidi kumalizia fedha zilizosalia mwezi mmoja baadae.

Mchango huo uliowasilishwa na jumuiya hiyo, ni moja kati ya jitihada zinazoendelea kufanywa  na mabalozi wa kampeni hiyo wenye kauli mbiu inayosema “Elimu yao wajibu wetu” kuhimiza wadau mbalimbali wa elimu kujitokeza na kuchangia ili kufanikisha ujenzi wa hosteli 30 zitakazogharimu jumla ya shilingi bilioni 2.3 bila samani.

.”Napenda kuwasilisha mchango huu kwa niaba ya wanafunzi wenzangu kwa kuonesha ni jinsi gani tumeguswa kwa namna ya pekee na kampeni hii kwani ujenzi wa hosteli hizo utasaidia kufanikisha elimu ya watoto wa kike nchini  na kukabiliana na matatizo yanayowakabili wanafunzi wa kike. Napenda kuwakumbusha kwamba huu ni mwanzo,kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo hivyo tutakavyoendelea kuchangia kwa hali na mali. Alisema Mwenyekiti huyo

Akipokea mchango huo Mkurugenzi Mkuu wa TEA  Bibi Rosemary Lulabuka amekishukuru kikundi hicho kwa  kujitolea kuchangia, ameeleza kuwa tatizo hili la ukosefu wa hosteli za wasichana umesababisha kushuka kwa kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa kike na hata kupunguza idadi  kutokana na kuongezeka kwa tatizo la  mimba, utoro na kupunguza maabukizi ya Ukimwi.

BiBI Lulabuka pia amewaomba wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni hii kwa kuchangia. Jumla ya shule 8 zitafaidika na hosteli hizo.


View Photo Gallery - (5)

Share this: