Jamani Foundation yatoa msaada wa madawati 150 kwa shule Tatu za Manispaa ya Ilala

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imepoke amchango wa madawati 150 kutoka Taasisi ya JAMANI (Jamani Foundation) kwa ajili ya shule za msingi tatu za manispaa ya Ilala. Shule zilizonufaika na msaada huo ni Umoja, Kigilagila na Muungano.

Msaada huo umewasilishwa na Meneja mkuu wa Jamani Foundation, ndugu Sadrudin Virji kwa niaba ya taasisi ya Jamani na Kupokelewa na Hamza Hassan ambaye ni Kaimu Meneja wa Uhamasishaji rasilimali wa Mamlaka ya Elimu Tanzania  kwa niaba ya shule tatu za manispaa ya Ilala. Hafla ya makabidhiano ya madawati hayo imefanyika Jumatano katika viwanja vya shule ya msingi Umoja iliyopo Kiwalani.

Msaada huu ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya ufadhili wa madawati 504 na vyoo kumi na mbili kuitoka Taasisi ya JAMANI (Jamani Foundation) kwa shule kumi na mbili za mkoa wa Dar es Salaam iliyotolewa tarehe 10. Machi. 2015. Thamani ya msaada huo ni  takribani shilingi milioni 65

Katika Uteuzi wa shule za kunufaika na msaada huu mkoani Dar es Salaam, Mamlaka ya Elimu Tanzania imezingatia mambo matatu, yaani; Ukubwa wa hitaji, ujirani kati ya shule na eneo analofanyia kazi mfadhili, na mapendekezo ya mfadhili.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014, nchi yetu inakabiliwa na upungufu wa madawati kwa asilimia arobaini na nne (44.4%). Yaani katika kila watoto kumi wanaoenda shuleni, wastani wa watoto zaidi ya wanne hawakai katika madawati.  Aidha kwa Mkoa wa Dar es salaam pekee, unaupungufu ni madawati yapatayo 67 elfu (kwa shule za msingi).