MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI (SDF) WAKOMBOA VIJANA KUTOKA KAYA MASKINI - ZANZIBAR

VIJANA 600 KUTOKA KAYA MASKINI WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UJUZI - ZANZIBAR


Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) kupitia Mpango wa Ufadhili kwa Vijana Kutoka Kaya Maskini na Wanaoishi Katika Mazingira Magumu (Bursary Scheme) umefanikiwa kunufaisha takribani vijana 600 kutoka katika visiwa vya Unguja na Pemba Zanzibar.

Akizungumza na maafisa wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Mwalimu Suleiman Zahoro kutoka Chuo cha Mafunzo ya Amali DAYA - Pemba alisema, mafunzo hayo ya ujuzi ni ukombozi kwa vijana wengi kutoka kaya maskini na walio katika mazingira magumu kwani yatawasaidia kujikwamua kiuchumi.


Mwalimu Zahoro ambaye ni mwalimu wa umeme wa magari ameelezea kufarijika na namna vijana walivyo na shauku ya kupata ujuzi baada ya kupata fursa ya kujiunga na mafunzo hayo.

"Vijana hawa wana bidii sana na shauku ya kutaka kujifunza bidii yao inatia moyo, alisema Mwl. Zahoro"

Kwa sasa vijana hao wanaendelelea na mafunzo kwa vitendo katika Chuo hicho cha Mafunzo ya amali DAYA kisiwani Pemba.

Nae Mussa Muhamed Juma mmoja kati ya vijana hao ambao wako kwenye mafunzo kwa vitendo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwakumbuka vijana wanaoishi katika mazingira magumu na kuwapatia mafunzo ya ujuzi bure, mafunzo ambayo wengi walikuwa wanayatamani lakini hawakuwa na uwezo wa kujigharimia.

Jumla ya vijana 600 wamenufaika na Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi (SDF) visiwani Unguja na Pemba kupitia Mpango wa Ufadhili kwa Vijana kutoka kaya maskini na wanaoishi katika mazingira unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Mafunzo hayo ya Kuendeleza Ujuzi kwa upande wa Pemba yalikuwa yanatolewa katika Vyuo vya Mafunzo ya Amali Vitongoji na DAYA pamoja na Kituo cha Elimu Mbadala Wingwi Mtemani.

TEA ilipewa jukumu la kusimamia na kutekeleza Mpango huo na Wizara Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuwafikia vijana kutoka makundi maalumu na wanaoishi katika mazingira magumu walio katika kaya zilizosajiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanafaidika na mpango huu kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujikwamua ki-uchumi na kujipatia kipato.