Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) Ashiriki Uzinduzi wa Jengo la Utawala Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST)

Pichani: Bi. Bahati Geuzye (Kushoto), akipokea zawadi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania kutoka kwa  Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Eng. Dkt Idrissa Muslim Hija (kulia).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye ameshiriki uzinduzi wa jengo la utawala la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) katika hafla iliyo fanyika katika viwanja vya KIST leo. Mgeni rasmi wa hafla hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Eng. Dkt Idrissa Muslim Hija.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi Geuzye amesema TEA imechangia jumla ya Shilingi Milioni Mia Mbili (Sh. 200,000,000) za Kitanzania kwaajili ya ukarabati na upanuzi wa jengo hilo. Aidha, Bi. Geuzye ameupongeza uongozi wa KIST kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha zilizotolewa chuoni hapo.  "Hizi ni fedha za umma, kwa maana ya kwamba zimechangiwa na Watanzania wote. Hivyo sisi kama Mamlaka ya Elimu nchini, tunayo furaha kubwa kuona kuwa uongozi wa Chuo hiki umesimamia vizuri matumizi ya fedha hizi na hivyo kuleta matumaini katika nchi yetu kuwa elimu bora inawezekana, endapo tutashirikiana pamoja kwa ufanisi na uzalendo."

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi Geuzye ameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ushirikiano ambao  TEA inaupata katika kuetekeleza miradi ya elimu inayofadhiliwa na TEA  Zanzibar. Amesema, TEA ni Taasisi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mamlaka ya Elimu Tanzania imepewa jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa. Mfuko huu una jukumu la kufadhili miradi ya elimu katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania Bara, na Elimu ya juu kwa Tanzania Zazibar, ambalo ni eneo muhimu la Muungano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akihutubia katika hafla hiyo, Bi. Geuzye amesema "TEA imeshiriki katika miradi ya ujenzi na upanuzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa na katika programu mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa elimu kwa usawa. Kwa mfano, kati ya Mwaka 2012 – 2016, Mamlaka ya Elimu Tanzania imefadhili programu ya kuwezesha watoto wa kike kufikia kiwango cha kudahiliwa kuchukua masomo ya sayansi katika elimu ya Juu. (Female Science Pre-Entry Program)." Bi Geuzye amesem Programu hiyo  iliwezesha watoto wa kike 594 kutoka Zanzibar kuingia katika programu za Sayansi katika vyuo mbalimbali nchini. Katika wanafunzi hawa, wanafunzi wa kike 345 walisoma katika Chuo cha KIST. 

Pia Mkurugenzi Mkuu amesema, katika kuboresha miradi ya Elimu Zanzibar, katika Mwaka huu wa fedha 2020/21, Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania tayari imeidhinisha kiasi cha Shilingi Milioni Mia Tatu (Sh.300,000,000/=) kwa chuo cha KIST kwa ajili ya kuendeleza ukarabati wa miundombinu na kuboresha zaidi mazingira ya kujifunza na kufundishia.