WADAU WA ELIMU WAHIMIZWA KUCHANGIA MFUKO WA ELIMU

 

WADAU WA ELIMU WAHIMIZWA KUCHANGIA MFUKO WA ELIMU

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye amewakumbusha wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi kutoa michango yao kupitia Mfuko wa Elimu unaoratibiwa na TEA ambao una jukumu la kisheria la kuratibu michango ya elimu nchini.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa mabati 500 kwa shule tano za msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Mkurugenzi Mkuu wa TEA amesema wadau wanapotoa misaada kupitia TEA wanasaidia Serikali kuratibu na kuingiza katika Kanzidata misaada hiyo, hivyo ameishukuru kampuni ya Yalin Global Company Limited ambayo ilitoa Mabati hayo kupitia Mfuko wa Elimu. “Kwa kuchangia kupitia Mfuko wa Elimu, Serikali inakuwa na takwimu sahihi na uratibu bora wa misaada ya elimu nchini”

Aidha wachangiaji wa Mfuko wa Elimu hupewa Cheti cha Utambuzi wa Mchango wa Elimu yaani “Certificate of Educational Appreciation”, ambacho kinamuwezesha mchangiaji kuomba kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) nafuu ya kodi ambayo inaweza kutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya Mwaka 2001 na Sheria ya Mapato ya Mwaka 2004.

Wakipokea msaada huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Bw. John John Nchimbi, amesema mabati hayo yatakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambao baadhi yao hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata elimu maeneo ya mbali, hivyo kupitia msaada huu, mabati hayo yataezeka madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Bw. Charles Lawiso amesema msaada huo utasaidia Manispaa kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa sasa kutokana na sera ya elimu bila malipo.

 Viongozi hao wa Halmashauri wameishukuru TEA kwa msaada huo ambao utaboresha miundombinu ya elimu katika maeneo yao.

Hafla fupi ya kukabidhi msaada wa mabati 500 yenye thamani ya Shilingi Milioni 12 imefanyika tarehe 31 Machi 2021 katika ofisi za Makao Makuu ya TEA zilizopo Mikocheni B Dar es Salaam ambapo shule tatu za msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Babati ya Mkoani Manyara yaani Maleshi, Majengo na Kazaroho na mbili kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ambazo ni Ugindoni na Raha Leo zimenufaika na msaada huo.