MFUKO WA ELIMU WA TAIFA WABORESHA UTOAJI WA ELIMU TAASISI YA KARUME YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (KIST)

MFUKO WA ELIMU WA TAIFA WABORESHA UTOAJI WA ELIMU TAASISI YA KARUME YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (KIST)

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Lela Mohammed Mussa amezindua jengo la Hanga litakalotumika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa uhandisi wa matengenezo ya ndege katika chuo cha Taasisi ya  Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) lililojengwa kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na kuipongeza  Serikali ya Jamhuri ya Muungano  kwa kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu katika Taasisi za Elimu ya juu za Tanzania Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mhe. Mohammed amesema ruzuku hiyo kiasi cha Sh. Milioni 300 iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TEA ni miongoni mwa matunda ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Mhe. Mussa ameongeza ujenzi wa Hanga utawezesha KIST kufuzu vigezo vinavyotakiwa katika utoaji wa mafunzo ya Uhandisi wa matengenezo ya ndege  kama inavyoelekezwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  ambayo ni mdhibiti wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya usafiri wa anga nchini.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa KIST, Dkt.  Mahmoud Abdoulwahab Alawi amesema ujenzi wa mradi huo wa Hanga ulianza Septemba 2021 na kukamilika Machi 2022 utatwezesha  wanafunzi  kupata mafunzo  ya matengenezo ya  ndege kwa vitendo.

Ameongeza kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa mafunzo  ya uhandisi wa ndege kwa wanafunzi 50 ambao wanatoka  Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Bi. Bahati I. Geuzye, amesema utoaji wa ruzuku katika chuo cha KIST ni sehemu ya majukumu ya Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na TEA kuongeza jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa.

Ameongeza kuwa TEA itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu katika taasisi za elimu ya juu za Tanzania Zanzibar ambapo amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kiasi cha Sh. Milioni 200 kimeelekezwa kwa Taasisi ya Utawala wa Umma Zanzibar (Institute of Public Administration-IPA).