WANAFUNZI WAHIMIZWA KUPENDA MASOMO YA SAYANSI

WANAFUNZI WAHIMIZWA KUPENDA MASOMO YA SAYANSI

Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula amewahimiza wanafunzi wa kitanzania kupenda masomo ya sayansi na teknolojia kutokana na mchango wake katika kuleta maendeleo ya nchi.

Prof. Kipanyula amesema Sayansi na Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa kitaifa na kimataifa na hasa katika sekta za elimu, habari, biashara na huduma mbali mbali za kijamii.

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika sekta ya elimu ambapo imewekeza kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hivyo kuwahamasisha wanafunzi kujifunza kwa bidii na kuwa wabunifu.

Alikuwa akizungumza katika hafla fupi ya kugawa majarida 700 yanayofahamika kama OYLA Africa ambayo yametolewa na kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam kufuatia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov  katika ofisi za TEA jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.

Bw. Semikov amesema lengo la Majarida hayo ni kuwezesha  wanafunzi wanaoyatumia kuwa wabunifu na wadadisi kwa lengo la kuboresha mazingira  na maisha yao kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye ameshukuru kampuni ya Baobab Shalom Limited kwa kutoa msaada huo  wa majarida kupitia Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA na kuongeza kuwa TEA iko tayari wakati wote kushirikiana na wadau wa elimu na kuwahakikishia kuwa misaada ya elimu inayopita kwenye  Mfuko wa Elimu wa Taifa inasimamiwa kikamilifu na kutumika kama ilivyokusudiwa.