BILIONI 8.9 KUTUMIKA KATIKA MIRADI YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI KATIKA MWAKA WA FEDAHA 2022- 2023.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepanga kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 8.9 kwa ajili ya kufadhili miradi ya  kuboresha miundombinu ya elimu nchini kupitia Mfuko wa Elimu wa taifa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kusaidia jitihada za Serikali katika kuwezesha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na   welekeo wa Bajeti ya TEA katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dar es Salaam tarehe Agosti 4, 2022.

 

Amefafanua kuwa kiasi hicho cha fedha kitatumika kujenga jumla ya miradi 96 katika shule za msingi na sekondari Tanzania bara pamoja na Taasisi mbili za elimu ya juu Tanzania Zanzibar.

 

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa madarasa 99, matundu ya vyoo 792, maabara 10 za masomo ya sayansi kwa ajili ya shule tano za sekondari, nyumba za walimu 52 na mabweni 10.

 

Miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inayojumuisha madarasa 10, matundu ya vyoo 40 pamoja na mabweni mawili katika shule sita zenye watoto wenye mahitaji maalum .

 

Ameongeza kuwa vigezo vinavyotumika kuchagua wanufaika wa ufadhili wa Mfuko wa Elimu ni pamoja na kuangalia shule zenye uhaba mkubwa wa miundombinu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi, usajili wa shule na orodha ya maombi ya ufadhili iliyoko kwenye kanzidata za TEA.

 

Katika mwaka wa fedha 2021/2022, kiasi cha Shs. Bilioni 8.8 zilitumika kugharimia ufadhili wa miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchin

Miradi hiyo ilijumlisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 70, Maabara 2 za sayansi katika shule za sekondari zenye mahitaji maalum, Matundu ya vyoo 1920 katika shule 80, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uendelezaji wa   miundombinu  katika shule  tisa za watoto wenye mahitaji maalum pamoja na ofisi mbili za walimu katika shule mbili.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TEA ameendelea kuhimiza wadau wa elimu kutoa  ufadhili  wa miradi ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa taifa ambao una jukumu la kisheria la kuratibu  michango  inayotolewa katika sekta ya  elimu nchini ili kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za  wachangiaji na thamani ya michango.

 

Taasisi au watu wanaochangia kupitia TEA wanatambuliwa rasmi kwa kupewa cheti maalum na wanaweza kuomba nafuu ya kodi kwa Kamishna wa Kodi ya Mapato Nchini (TRA). Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mapato ya mwaka 2006.

 

Kuhusu  utekelezaji wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), Mkurugenzi Mkuu wa TEA amesema hadi kufikia mwezi Juni 2022 kiasi cha Shs   Bilioni 8.6 zimetolewa kwa ajili ya kufadhili miradi 81 ambapo  jumla ua wanufaika 33,510 ikiwa ni wanaume 17,257 (51.5%) na wanawake 16,253 (48.5%) wamepatiwa mafunzo.

 

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.