KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA ATEMBELEA TEA

 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Micheal leo tarehe 21 Julai, 2022 amekutana na kuzungumza na watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) alipofanya ziara ya siku moja katika Makao Makuu ya TEA Mikocheni jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuangalia  zinavyotekeleza majukumu yake.

 

Akizungumza na watumishi wa TEA, Dkt. Micheal amesema, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inatoa kipaumbele  katika sekta ya elimu kwa kuwekeza fedha nyingi za kuendeleza sekta hiyo, hivyo watumishi wa  TEA wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa weledi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha sekta ya elimu.

 

Ameongeza kuwa kwasasa Serikali inaweka msukumo katika  elimu  ya  mafunzo ya kukuza ujuzi kwa lengo la kuwezesha vijana wakitanzania kujitegemea pindi wanapohitimu masomo.

 

Dkt. Micheal pia ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa Mamlaka  ya Elimu Tanzania kuwa wanawajibu wa kuwatumikia wananchi kwa vile ni wajibu wa viongozi kuwatumikia  walio chini yao.

 

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.