TEA YASHIRIKI MAONYESHO YA ELIMU YA UFUNDI NA UFUNDI STADI JIJINI DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka  leo tarehe 7 Juni 2022 ametembelea Banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika maonyesho ya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi, yanayoendelea katika Viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma.

Maonyesho hayo ya wiki moja ambayo yameandaliwa na  Baraza laTaifa la  Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVET) yamenza leo jijini Dodoma na yanatarajiwa kufunguliwa Rasmi, Tarehe 10 Juni 2022 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Phillip Isdor Mpango.

TEA inashiriki maonyesho hayo kutokana na kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ambao unatoa ufadhili wa Mafunzo ya kuendeleza Ujuzi na stadi za kazi kwa vijana wa kitanzania. Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na SDF yanajikita kwenye sekta sita za kipaumbele ambazo ni  Kilimo na Kilimo Biashara, Utalii na Huduma za Ukarimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), Ujenzi, Nishati na Uchukuzi.

 

Zaidi ya vijana 32,000 wamenufaika na ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza ujuzi unaoratibiwa na TEA ili kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. Katika awamu ya kwanza ya mradi ulioanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.1 wakati katika awamu ya pili Taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.