Utafutaji Rasilimali Kwa Ajili ya Ufadhili Wa Elimu
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inasimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa. Mojawapo ya majukumu ya msingi ya TEA ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa ili kuongeza nguvu katika juhudi za Serikali za kufadhili miradi ya elimu katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na ngazi ya elimu ya juu Tanzania Zanzibar. Jukumu hili linahitaji dhamira na ushirikiano wa wadau wa elimu kutoka sekta ya umma na sekta binafsi.
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Tanzania imepata mafanikio mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa. Tathmini ya Mpango wa Sekta ya Elimu wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021, iliyofanyika mwaka 2018 kuhusu utekelezaji wa sera mbalimbali za elimu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ilibainisha kuwa sekta ya elimu imekua kwa kasi katika ngazi zote.
Kwa mfano, mwaka 2017, kiwango halisi cha uandikishaji wa watoto katika elimu ya awali kilifikia asilimia 44.6, kiwango ambacho kilikuwa miongoni mwa viwango vya juu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kiwango cha jumla cha uandikishaji katika elimu ya msingi kilikaribia kufikia asilimia 100, kikiwa asilimia 96.9. Aidha, zaidi ya asilimia 70 ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi huendelea na elimu ya sekondari.
Elimu ya juu nayo imepanuka kwa kasi, kutoka taasisi zisizozidi 20 mwaka 2005 hadi zaidi ya taasisi 50 mwaka 2016. Katika kipindi hicho, idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika elimu ya juu iliongezeka zaidi ya mara nne, kutoka chini ya 40,000 mwaka 2005 hadi zaidi ya 200,000 mwaka 2015.
Licha ya mafanikio hayo katika kupanua upatikanaji wa elimu katika ngazi mbalimbali, bado kuna changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya elimu nchini Tanzania. Changamoto kuu ni upungufu na hali duni ya miundombinu ya elimu, hasa katika elimu ya msingi na sekondari ya chini, pamoja na ukosefu wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya kujenga miundombinu inayohitajika na kuboresha vifaa vya kufundishia na kujifunzia, hususan katika maeneo ya vijijini.
Changamoto hizi zimeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto wanaopata elimu ya msingi, pamoja na uwezo wa wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu wa kujifunza na kuendeleza maarifa na ujuzi katika maisha yao yote.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeongeza mgao wa bajeti ya matumizi kwa sekta ya elimu hadi zaidi ya asilimia 21 ya matumizi ya Serikali, huku mgao unaotengwa kwa elimu ya awali na msingi ukiendelea kuwa zaidi ya asilimia 50 na kuonyesha mwelekeo wa kuongezeka.
Hata hivyo, ili kufikia lengo la kuwa na jamii iliyoelimika, rasilimali zaidi kutoka katika taasisi za umma na binafsi zinahitajika. Hivyo, wadau na taasisi mbalimbali zinazoweza kuchangia zinahimizwa kushiriki katika kuboresha upatikanaji wa elimu kwa usawa.
NANI ANAWEZA KUCHANGIA?
Kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)(a) na (b) cha Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001, mchangiaji ni mtu yeyote anayetoa mchango wa fedha, bidhaa na/au huduma kwa Mfuko wa Elimu a Taifa au mradi unaofadhiliwa na Mfuko huo.
Aidha, mchangiaji anaweza kuwa mtu anayetoa ufadhili au ruzuku kwa wanafunzi ambao si watoto wake, wanafamilia wake au wafanyakazi wake, kwa lengo la kuwawezesha kupata elimu ya sekondari au elimu ya juu.
Wachangiaji wa Mfuko wa Elimu wanaweza kuwa:
- Watu binafsi;
- Mashirika na kampuni;
- Taasisi za umma na binafsi;
- Mashirika ya kiraia; na
- Taasisi za kidini.
AINA ZA MICHANGO INAYOKUBALIWA
Michango inayoweza kupokelewa na Mfuko wa Elimu ni pamoja na:
1. Michango ya fedha
Michango ya fedha hupokelewa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Malipo ya Serikali (Government Electronic Payment Gateway – GePG).
2. Michango isiyo ya fedha
Michango hii inajumuisha bidhaa, mali na huduma zinazotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu au miradi inayofadhiliwa na Mfuko huo.
MOTISHA KWA WACHANGIAJI
Kila mchangiaji wa Mfuko wa Elimu anastahili kupata manufaa yafuatayo:
(i) Kutambuliwa na kuthaminiwa
Mchangiaji wa Mfuko wa Elimu hutunukiwa Cheti cha Shukrani kwa Mchango wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation – CEA) au Barua ya Shukrani kwa Mchango wa Elimu (Letter of Education Appreciation – LEA) kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake katika maendeleo ya elimu.
Wachangiaji wanaotoa zaidi ya Shilingi 50,000 kwa watu binafsi au wafanyakazi, au zaidi ya Shilingi 100,000 kwa mashirika, kampuni, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kiraia na taasisi za kidini, wanastahili kupata Cheti cha Shukrani kwa Mchango wa Elimu.
Rangi ya Cheti cha Shukrani kwa Mchango wa Elimu hutegemea thamani ya mchango uliopokelewa kama ifuatavyo:
- Bluu ya Metali (Metallic Blue): Shilingi 100,000 hadi 999,999.
- Fedha ya Metali (Metallic Silver): Shilingi 1,000,000 hadi 9,999,999.
- Nyekundu ya Metali (Metallic Red): Shilingi 10,000,000 hadi 99,999,999.
- Dhahabu ya Metali (Metallic Gold): Shilingi 100,000,000 na zaidi.
(ii) Nafuu ya kodi
Wachangiaji wanaolipa kodi wanaweza kuomba kupatiwa nafuu ya Kodi ya Mapato, kwa kuwasilisha Cheti cha Shukrani kwa Mchango wa Elimu kilichosainiwa katika ofisi husika ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wapokeaji wote wa Vyeti vya Shukrani kwa Mchango wa Elimu wana haki ya kuwasilisha maombi ya nafuu hiyo ya kodi, kwa kuzingatia taratibu na masharti yanayotumika.
(iii) Usajili
Kila mchangiaji atasajiliwa katika Daftari la Wachangiaji wa Mfuko wa Elimu kwa ajili ya kumbukumbu za kudumu za mchango wake katika maendeleo ya elimu nchini.