The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

WITO WA MAOMBI YA RUZUKU YA KUENDELEZA UJUZI KATIKA NYANJA ZAMAFUNZO YA KIUBUNIFUKWA NJIA YAELIMU MTANDAO (E-LEARNING DELIVERY MODE) KUPITIA MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI (SKILLS DEVELOPMENT FUND- SDF)

 

Utangulizi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) inaendelea na utekelezaji wa Programu mbalimbali lengo likiwa ni kufikia uchumi wa juu wa kati (Upper Middle Income Country) na Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Aidha, katika kufanikisha azma hii, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wanatekeleza Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs-ESPJ). Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Ujuzi (National Skills Development Strategy - NSDS), na unalenga kuongeza fursa za ajira katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni: Kilimo, Kilimo – Biashara na Uchakataji wa Mazao ya kilimo; Utalii na Huduma za Ukarimu; Uchukuzi; Ujenzi; Nishati; na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imekasimiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) jukumu la kusimamia utekelezaji wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi ambao upo chini ya Programu ya ESPJ. Aidha Dirisha la Mafunzo ya Kiubunifu kwa njia ya Mtandao ni sehemu ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).

Katika kuhakikisha tunafikia malengo ya utekelezaji wa Dirisha hili, Mamlaka ya Elimu Tanzania imetenga fedha kwa ajili ya kugharamia Ubunifu katika kutoa Mafunzo ya kuendeleza Ujuzi kwa njia ya Mtandao. Maudhui ya Programu za mafunzo ya kiubunifu ni sharti yawekwe wazi (Public Domain) ili kuruhusu umma wote kuweza kujifunza kwa madhumuni ya uendelevu wa upatikanaji wa ujuzi.

Hivyo, Taasisi zinaalikwa kuwasilisha maandiko ya miradi ili kuomba Ruzuku kwa ajili ya:

  1. Miradi ya kiubunifu kama vile matumizi ya Teknolojia za kidijitali kuwezesha kutoa mafunzo (mfano: madarasa yenye kutumia TEHAMA (smart classrooms, computers for simulations etc.);
  2. Kuanzisha mafunzo mapya ya programu za kiubunifu kwa njia ya Elimu Mtandao (e-learning delivery mode) yanayolenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya ujuzi wa kidigitali;
  3. Kuimarisha programu zilizopo kwa kuhuisha maudhui ya kiubunifu; na
  4. Kuimarisha mafunzo ya kiubunifu kwa njia ya Elimu Mtandao ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupata mafunzo kwa gharama nafuu.

Maeneo ya Ufadhili

Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, TEA kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi, imetenga fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya kiubunifu ya kuendeleza ujuzi kwa Njia ya Mtandao. Fedha itakayotolewa ilenge kutekeleza mambo yafuatayo:

Sekta

Teknolojia Mpya/ Bunifu

Kilimo na Kilimo Biashara

  • Maendeleo ya Viumbe hai
  • Teknolojia ya Vitalu-nyumba
  • Ufugaji Mchanganyiko wa Samaki na Mbogamboga
  • Teknolojia ya Mifugo
  • Usalama na Utunzaji wa Chakula
  • Ufuatiliaji wa Mazao Kidijitali
  • Kilimo cha Kiteknolojia
  • Kilimo cha Kiteknolojia kuzingatia Hali ya Hewa

Ujenzi

  • Teknolojia inayoongeza Ubora, kupunguza gharama, kupunguza ajali, na kuongeza ufanisi kukamilisha ujenzi kwa wakati
  • Makazi endelevu yanayotumia nishati kidogo
  • Matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo rafiki wa mazingira
  • Matumizi ya teknolojia ya Computerized Numerical Control (CNC) katika kazi ya usanifu na uhandisi

Utalii na Huduma za Ukarimu

  • Utalii wa Mazingira
  • Utalii wa kijamii
  • Utalii wa matukio

Uzalishaji

  • Mafunzo ya Teknolojia ya CNC kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na ushindani katika soko, mfano: Uchomeleaji, utengenezaji samani n.k.

Usafirishaji na Uchukuzi

  • Kozi za ufundi wa kiteknolojia wa magari kwa kutumia Teknolojia ya CNC
  • Utatuzi wa Matatizo ya Kiufundi katika Magari kwa njia ya Kompyuta
  • Kozi zitakazobadili tabia za Madereva Wataalamu na kupunguza ajali
  • Kozi zitakazoongeza huduma za usimamizi wa mizigo, kwa kutumia TEHAMA

Nishati

  • Masomo yanayohusiana na matumizi ya teknolojia ya jua
  • Ujenzi na Uzalishaji wa Mifumo ya gesi ya kibaolojia
  • Teknolojia ya usimamizi wa maji

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)

  • Kozi ya Awali ya TEHAMA kwa makundi maalumu kama vile mafundi wa  magari, wafanyabiashara ndogondogo wasio rasmi na wanawake vijijini
  • Zana za kujifunzia kidijitali katika madarasa
  • Uuzaji wa kidijitali kupitia mitandao ya kijamii kama vile; FacebookInstagram, WhatsApp, mauzo ya mtandaoni n.k.
  • Kupambana na Uhalifu-Mtandao
  • Uundaji wa mifumo - kuunda tovuti, matumizi ya programu
  • Mfumo ulioungwa Vifaa vya TEHAMA
  • Kuanzishwa kwa teknolojia za kidijitali kama vile Computerized Numerical Control CNC na Programmable Logic Controller (PLC) katika programu za mafunzo ya Ufundi na Elimu ya Ufundi Stadi
  • Akili Bandia za Kidijitali
  • Kujifunza kwa njia ya Mtandao na kujifunza kwa Mseto (blended learning) ikijumuisha ununuzi na uendelezaji wa kozi za kujifunzia mtandaoni kwa mafunzo ya Ufundi na Elimu ya Ufundi Stadi, Ununuzi wa vifaa kwa ajili ya taasisi za mafunzo ya Ufundi na Elimu ya Ufundi Stadi kwa ajili ya kuanzisha kozi za mtandaoni, Mafunzo ya Ualimu kwa kutumia mbinu za ufundishaji kwa njia ya mtandao
  • Biashara ya kielektroniki
  • Matumizi ya Simu-janja na programu za Simu kwa ajili ya kuongeza ufikiaji wa huduma/fursa zinazopatikana
  • Ukuzaji wa haraka wa programu za tovuti na zinazotegemea simu kwa kutumia vyanzo/teknolojia huria
  • Ukarabati na matengenezo ya simu kwa kutumia teknolojia ya multimedia/video
  • Kukuza maendeleo, kujumuisha na matumizi ya huduma za eneo katika kuboresha huduma za usafiri, Matumizi ya Blockchain na teknolojia nyingine mahiri hasa katika sekta sita za kipaumbele za ESPJ
  • Eneo lingine lolote la ukuzaji ujuzi ambalo litachangia katika kukuza uchumi wa kidijitali huku likiongeza nafasi za ajira

 

Vigezo vya Kuchaguliwa

Vigezo vifuatavyo vitatumika katika mchakato wa uchaguzi wa Taasisi zitakazonufaika:

  1. Mafunzo lazima yawe ya kiubunifu katika ngazi ya Taifa, na yawe na mchango katika maendeleo ya uchumi ya Taifa.
  2. Mafunzo lazima yaendane na mahitaji ya ujuzi husika katika soko la ajira, ikiwemo waajiri.
  3. Mafunzo yaweze kuvutia idadi kubwa ya wanufaika watakaohitaji kujifunzia.  
  4. Kipaumbele kitatolewa kwa miradi ya kiubunifu kama vile matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika kutoa mafunzo katika darasa la ki-TEHAMA (smart classrooms, computers for simulations etc.)
  5. Uwezo wa kuanzisha kozi mpya ambazo zinazolenga kutatua changamoto ya kuongezeka   kwa mahitaji ya ujuzi wa Kidijitali kwa Wananchi.
  6. Taasisi iwe imesajiliwa kisheria, pia iwe na Mpango endelevu wa mafunzo haya.

Walengwa wa Mafunzo

Mafunzo haya yamelenga kuwanufaisha jumla ya Watanzania (vijana) 4350 nchi nzima ili waweze kuongeza tija katika shughuli zao za kawaida za uzalishaji mali kulingana na mahitaji ya nchi kwenye sekta za kipaumbele.

Sifa za Waombaji

Taasisi zinazokidhi vigezo vifuatavyo zinaweza kuomba ruzuku:

  1. Taasisi za ngazi ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Technical Colleges and Vocational Training Institutions) zinazotoa mafunzo katika sekta sita za kipaumbele za ESPJ, ambazo zimesajiliwa na zinatambulika kisheria. Vyuo Vikuu havipaswi kuomba;
  2. Taasisi iwe na uwezo wa kuendeleza na kuendesha shughuli za Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi kwa njia ya Elimu Mtandao hata baada ya ufadhili wa SDF kufikia ukomo (Mpango kazi Endelevu Uwasilishwe);
  3. Taasisi iwe na rekodi za uadilifu katika matumizi ya fedha za umma na ukamilishaji kwa wakati na ubora unaotakiwa wa miradi waliyowahi kutekeleza na kipaumbele kitatolewa kwa Taasisi zilizotekeleza kwa ufanisi miradi ya awamu ya kwanza na ya pili ya SDF.

Namna ya Uendeshaji wa Mafunzo

  1. Mafunzo ya kiubunifu kwa njia ya Elimu Mtandao yalenge katika sekta sita za kipaumbele kama zilivyoainishwa katika sehemu ya Utangulizi wa tangazo hili;
  2. Mafunzo yatolewe kati ya mwezi mmoja na miezi mitatu na yalenge kutatua changamoto za ujuzi katika sekta husika. Aidha, Taasisi itakayotoa mafunzo ihakikishe programu inapatiwa ithibati kutoka Mamlaka husika;
  3. Jukwaa la mafunzo (Training Platform) litambuliwe rasmi na Mamlaka ya Taasisi husika na kuhakikiwa na timu ya wataalamu wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF);
  4. Programu zitakazopatiwa ruzuku ziwe na uwezo wa kutoa mafunzo kwa vijana wasiopungua 270 kwa Taasisi za ngazi ya Ufundi na 300 kwa Taasisi za ngazi ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na
  5. Mafunzo yazingatie makundi maalum ya wanawake na watu wenye walemavu. Inashauriwa angalau asilimia 45 ya Washiriki wawe ni wanawake.

Ruzuku Iliyotengwa

Fedha kiasi cha Shillingi (TZS) 131,220,000/= zimetengwa kwa kila Programu itakayoombwa na Taasisi. Aidha, Taasisi inashauriwa kuomba ruzuku kwa ajili ya Programu moja ya mafunzo itakayonufaisha Wanufaika wasiopungua 270 kwa Vyuo vya Ufundi au 300 kwa Vyuo vya Ufundi Stadi. Ruzuku hii inalenga kufadhili Vyuo 5 vya Ufundi na Vyuo 10 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Namna ya Kupata Ruzuku

  1. Waombaji watawasilisha maandiko ya Miradi na yatapitiwa ili kubaini kama yanakidhi vigezo vya kupatiwa Ruzuku. Aidha Taasisi zitakazokidhi vigezo vya awali zitatembelewa ili kuhakiki uhalisia wa taarifa zilizowasilishwa katika maandiko. Baada ya timu ya wataalamu kujiridhisha, Taasisi hizo zitapatiwa Ruzuku baada ya kusaini Mkataba wa Ruzuku na utekelezaji wa Mradi.  
  2. Mwongozo wa jinsi ya kuomba ruzuku hii unapatikana katika kwenye Tovuti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (www.tea.or.tz) sehemu ya matangazo.

 

Muda na Namna ya Kutuma Maombi

Maombi yote yaandaliwe kwa kufuata Mwongozo uliotolewa na TEA. Mwongozo huo unapatikana katika Tovuti ya TEA (www.tea.or.tz) sehemu ya matangazo au unaweza kuombwa kwa njia ya barua pepe kupitia: sdf@tea.or.tz au kuchukua nakala Ofisi za TEA.

Muda wa kuwasilisha maombi ni siku 14 kuanzia tarehe 11 Aprili 2022na mwisho ni tarehe 25 Aprili 2022.Baada ya tarehe ya mwisho, hakuna Maombi yatakayopokelewa. Maombi yote yatumwe kwa njia ya huduma ya kasi ya vifurushi (speed courier mail) kama vile EMS, DHL au nyinginezo. Maombi hayo yatumwe kwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa Anwani inayoonekana mwishoni mwa Tangazo hili.

Taasisi inayotuma maombi iwasilishe nakala tatu (3) za Maombi yao, zikiambatana na Barua ya kuwasilisha maombi na kuambatisha nyaraka zote stahiki zinazohitajika. Maombi ambayo hayatakuwa na nyaraka zinazohitajika hayatafanyiwa kazi.

Taarifa kwa Umma Kuhusu Orodha ya Waombaji Watakaopatiwa Ufadhili

Orodha ya waombaji watakaofanikiwa kupatiwa ufadhili itatangazwa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano kwa Umma. Hata hivyo, Taasisi husika itajulishwa kwa barua rasmi. Halikadhalika waombaji wasiofanikiwa watajulishwa kupitia barua pepe zao.

Maulizo na Mawasiliano kuhusu wito huu

Kwa maulizo na mawasiliano zaidi wasiliana  nasi kwa  Namba ya simu ya ofisi: +255 22 2781165, au Mratibu wa SDF (+255789304181 au +255754304181)  au barua pepe: masozi.nyirenda@tea.or.tz au sdf@tea.or.tz

Uwasilishaji wa Malalamiko

Waombaji wa ufadhili kama watakuwa na malalamiko yoyote kuhusu ufadhili huu watapaswa kuyawasilisha kwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa anwani iliyooneshwa hapo chini:

 

                                        

Mkurugenzi Mkuu,

Mamlaka ya Elimu Tanzania,

Kiwanja Na. 711/1, Barabara ya Bima,

Mikocheni B,

S.L.P. 34578,

DAR ES SALAAM.

Barua pepe: info@tea.or.tz

Simu:+255 22 2781165 | +255 22 2781079
Nukushi:+255 22 2781086