Published at: Thu, Dec 7, 2023 4:55 PM
Shirika la Camara Education Tanzania limetoa msaada wa Kompyuta 100 zenye thamani ya Sh. Milioni 37 kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ina jukumu la kisheria la kukusanya michango kwa ajili ya sekta ya elimu nchini.
Kompyuta hizo 100 zimetolewa kwa shule nne za Sekondari zilizoko kwenye Mikoa ya Tanga na Pwani ambapo kila shule imepata Kompyuta 25 kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kupata masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kompyuta hizo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Semkiwa Wilayani Korogwe Mkoani Tanga tarehe 23 Agosti 2023, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Jokate Mwegelo amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii kutokana na kuwekewa mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.
“Namna pekee mnyoweza kuonyesha shukrani kwa wafadhili walioleta msaada shuleni kwenu ni kusoma kwa bidii na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yenu”. Amesema Mkuu wa Wilaya ya Korogwe.
Katika hafla hiyo, shule ya Sekondari Semkiwa ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Shule ya Sekondari Kwaluguru ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni zimekabidhiwa Kompyuta 25 kila moja.
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani wanufaika ni Shule ya Sekondari Rafsanjani Soga iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha na Shule ya Sekondari Simbani iliyopo katika Halmashauri ya Kibaha ambapo kila shule itapata Kompyuta 25.
Mwakilishi wa Camara Education Tanzania, Bi. Asia Bonanga amesema shirika la Camara Education Tanzania, linajikita katika kupeleka teknolojia ya mawasiliano mashuleni ili kusaidia jitihada za kupatikana kwa elimu bora nchini.
Ameongeza kuwa maono ya Camara Education Tanzania ambalo ni kuona hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano - TEHAMA.
Kaimu Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Raslimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA, Bw. Masozi Nyirenda ameshukuru Shirika la Camara Education Tanzania kwa msaada huo wa Kompyuta na kukumbusha shule zilizonufaika kuzitumia na kuzitunza vizuri ili zidumu na kunufaisha kundi kubwa la wanafunzi.
“Kama tunavyofahamu vifaa hivi vinahitaji utunzaji maalum ikiwa ni pamoja na kuwa na vyumba vinavyofaa, hivyo shule nufaika zijiandae vyema kwa hili” ameongeza Bw. Nyirenda.
TEA ni Taasisi ya umma inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo kupitia Mfuko wa Elimu wa taifa inafadhili ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, mabweni, mabwalo na majiko yake, maabara na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na ngazi ya Elimu ya Juu.