The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

MILIONI 200 ZATUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU KATIKA JIJI LA MBEYA

Published at: Thu, Dec 7, 2023 3:34 PM

Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) umetumia Shilingi Milioni 200 kuboresha miundombinu ya Elimu ya Msingi katika jiji la Mbeya katika mwaka wa fedha wa 2021/ 2022 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha upatikanaji wa elimu bora nchini.

Haya yamebainishwa wakati wa ziara ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika miradi miwili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu wa Taifa katika shule za Msingi za Iganjo na Iwambi za jijini Mbeya.

Kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, unaoratibiwa na TEA, Shule ya Msingi Iganjo imepata ufadhili wa Shilingi milioni 100 ambazo zimegharimia ujenzi wa madarasa matatu, ofisi moja ya walimu na matundu 28 ya vyoo.

Katika Shule ya Msingi Iwambi mfuko umetoa ufadhili wa Shilingi milioni 100 zilizotumika kujenga madarasa matatu, ofisi moja ya walimu na matundu 24 ya vyoo. Karibu wanafunzi elfu nne wanaosoma katika shule hizo mbili wamenufaika na  ufadhili huo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini ambako miradi hiyo imetekelezwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha  za Mfuko wa Elimu wa Taifa ambazo zinatumuika kuboresha miundombinu ya elimu katika sehemu mbali mbali nchini ikiwa ni pamoja na  Mbeya.

Awali akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/22 Shilingi bilioni 8.8 zimetumika  kufadhili miradi ambayo ni pamoja na ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kujifunza na kufundishia.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko Mfuko wa Elimu Taifa   ambao unaongeza jitihada za Serikali  katika  kuboresha miundombinu ya elimu nchini kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa