Published at: Wed, Apr 24, 2024 11:06 AM
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha leo amekutana na wajumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa majukumu na mipango ya TEA katika kutoa huduma kwa umma kupitia ufadhili wa miundombinu ya elimu.
Mkutano huo uliofanyika kupitia uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika ukumbi wa mikutano wa NSSF Mavuno House Ilala Dar es Salaam ni sehemu ya jitihada za Serikali kuelezea huduma inazozitoa kwa wananchi kupitia taasisi zake.
Akizugumza katika mkutano huo, Dkt. Kipesha amesema moja ya majukumu ya TEA ni utafutaji rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na kwamba njia mojawapo inayotumika katika jitihada hizo ni uandaaji wa maandiko ya miradi yatakayowezesha kupata fedha kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi ili kusaidia uendelezaji wa miundombinu ya elimu.
Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2022/2023 jumla ya michango na ufadhili waSh.1.4imekusanywa kutoka kwa wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Asilia Giving inayojihusisha na shuguli za utalii Jijini Arusha pamoja na Taasisi ya Flaviana Matata.
Mkurugenzi MKuu wa TEA ametaja faida za mchangiaji wa maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu kuwa ni pamoja na kupata Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation) kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001.
Faida nyingine ni kupata nafuu ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya mwaka 2019 pamoja na kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu.
Aidha katika mkutano huo wahariri wameelezwa kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Mamlaka ya Elimu Tanzania imepanga kufadhili jumla ya miradi 82 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za Msingi na Sekondari kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Miradi hii itakapokamilika itanufaisha wanafunzi 39,484 na walimu 169 katika shule za msingi na sekondari nchini.
Miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32.