Published at: Thu, Jul 31, 2025 4:20 PM
Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Dkt. Leonard Akwilapo atembelea banda la TEA maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), na kusema TEA imejipanga kutekeleza miradi ya Amali
''Sisi kama Mamlaka ya Elimu Tanzania tumepewa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya mafunzo ya amali katika shule zilizoteuliwa kutoa mafunzo hayo,'' alisema Dkt. Akwilapo.
Dkt. Akwilapo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la TEA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipatia TEA fedha kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu.
Alibainisha kuwa TEA itaendelea kufadhili miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo nchini, ili kuimarisha ubora wa elimu ya vitendo.
Vilevile, Dkt. Akwilapo alizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na kusimamiwa na TEA, ambao umewawezesha maelfu ya vijana kupata mafunzo yanayowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato.
Akiwa katika banda la TEA, alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo waliofadhiliwa kupitia SDF, ambao walieleza namna mafunzo hayo yalivyobadilisha maisha yao.
TEA ilishiriki Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, pamoja na kujenga mahusiano na wadau muhimu ili kuimarisha ushirikiano wa kikazi.