Published at: Thu, Dec 7, 2023 3:08 PM
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha ametunuku hati za utambuzi wa elimu kwa taasisi 18 nchini zilizochangia maendeleo ya elimu kupitia mamlaka ya Elimu Tanzania.Katika hafla hiyo, zilizotunukiwa hati hizo za utambuzi wa elimu ni; Oxford University Press, Plan International, Avanti Communications Plc, Camara Education Tanzania, Uk Space Agency, Sunshine Company Ltd, Open Unuversity Of Tanzania, Jamani Foundation, Ucsaf, Tanzania Revenue Authority, Darsh Industries, United Bank Of Africa (Uba), Crdb Bank, Kcb Bank, Total Tanzania Ltd, Sight Savers, Social Action Trust Fund na , Tanzania Communications Regulatory Authority (TCRA).
Mhe. William Ole Nasha amesema Serikali inatambua mchango wa wahisani na wadau wa Elimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika kuendelea kuchangia ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi wa kike, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Naibu Waziri Ole Nasha amewahakikishia wahisani hao usalama wa fedha zao na kuwa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. “Niwahakikishie kuwa Serikali inatambua mchango wenu katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchangia Elimu, ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi wa kike, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum,”
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania Prof. Maurice Mbago ametoa shukrani za dhati kwa wachangiaji hao, na ameziomba Taasisi hizo ziendelee kuchangia maendeleo ya elimu kupitia TEA, na kuziomba taasisi nyingine ziendelee kuchangia kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA.