Published at: Wed, Nov 13, 2024 4:31 PM
Dodoma
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la AKO Tanzania Community Support lenye makao yake Mkoani Kilimanjaro limeonyesha nia ya kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamia na Mamlaka ya Elimu Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bi. Hilda Kimath ameonyesha nia hiyo alipomtembelea Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha ofisini kwake Ilazo Extension Jijini Dodoma tarehe 8 Novemba 2024 kuona jinsi wanavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya Elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Bi. Kimath amesema, shirika lao limejikita kufanya miradi kama inayofanywa na Mfuko wa Elimu wa Taifa hivyo ni vyema wakaunganisha nguvu na Mfuko huu unaosimamiwa na TEA ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi zaidi.
‘‘Naamini tukitekeleza hii miradi kwa pamoja, tutakuwa na uhakika wa usimamizi lakini pia kuinua ubora wa miradi tunayotekeleza kwani TEA ambayo ni Shirika ni Serikali ina uzoefu wa kufanya miradi kama hii amesema” Bi Hilda.
Ameongeza kuwa, wakati mwingine shirika lake linakabiliwa na changamoto ya kutokamilisha miradi yake kwa wakati au kutumia gharama kubwa hivyo anaamini ushirikiano wake na TEA ambayo tayari ina uzoefu na miungozo maalum ya utekelezaji wa miradi utasaidia kupunguza changamoto.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha amelishukuru shirika hilo na kusema ana farijika kuona wadau wanachangia maendeleo ya Elimu na kwamba TEA ipo tayari kufanya kazi na wadau wote wa elimu ili kuinua kiwango cha ubora wa elimu na kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaboreshwa.
Ametaja faida watakazopata wadau wanaochangia maendeleo ya Elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasimamiwa na TEA kuwa ni pamoja na kutambuliwa kitaifa kwa kuingizwa kwenye orodha ya wachangiaji wa elimu, kupewa Cheti cha utambuzi kama mchangiaji wa Elimu na kwamba mdau anaweza kutumia cheti hicho kuomba nafuu ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa, wenye lengo la kuongeza nguvu za Serikali kugharamia miradi ya elimu ili kuinua upatikanaji wa elimu bora kwa usawa katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania Bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar.