The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

TEA KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LA BRAC- MAENDELEO TANZANIA KATIKA KUBORESHA ELIMU NCHINI

Published at: Thu, Dec 7, 2023 3:21 PM

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Shirika lisilo la Kiserikali la BRAC - Maendeleo Tanzania leo tarehe 10 Februari 2022 wameingia Makubaliano maalum ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi inayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia nchini.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bi. Bahati I. Geuzye na Mkurugenzi Mwakilishi wa BRAC - Maendeleo Tanzania, Bi. Susan Bipa, katika Makao Makuu ya TEA, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Kupitia makubaliano haya Shirika la BRAC - Maendeleo Tanzania litatoa ufadhili wa miradi ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA. Kwa kuanzia Shirika la BRAC -Maendeleo Tanzania limepanga kutoa Kompyuta 120 zenye thamani ya Shilingi 132,600,000 katika shule tatu za Sekondari za Miburani, Wailes na Karibuni zilizopo Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam. Wanafunzi 600 na walimu 26 watanufaika na ufadhili huo.

Mamlaka ya Elimu Tanzania, imekuwa ikihimiza wadau wa elimu kutoa ufadhili wa miradi ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao una jukumu la kisheria la kuratibu michango inayotolewa katika Sekta ya Elimu nchini ili kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za wachangiaji na thamani ya michango.

Taasisi au watu wanaochangia kupitia TEA wanatambuliwa rasmi kwa kupewa cheti maalum na wanaweza kuomba nafuu ya kodi kwa Kamishna wa Kodi ya Mapato Nchini (TRA). Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mapato ya mwaka 2006.

 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.