The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

TEA na UNICEF Tanzania zakutana kutathmini utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya elimu

Published at: Sat, Oct 26, 2024 2:30 PM

Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Oktoba 24, 2024 imekutana na Mhandisi wa miradi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Mhandisi Mohamed Hindi, kujadili utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa shule 13 katika mikoa ya Kigoma, Tabora, na Songwe. Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhili wa UNICEF kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa

Katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya TEA, Ilazo, Jijini Dodoma, pande zote mbili zimepitia utekelezaji wa mradi huo ulioanza Julai 2024 na kudumu kwa miezi mitatu. Tathmini hiyo imebainisha mafanikio na changamoto zilizojitokeza, huku ikijadiliwa mbinu bora za kutatua changamoto hizo.

Akizungumza katika tathmini hiyo, Mhandisi Hindi alisema kuwa mradi huo umelenga kukabiliana na upungufu wa maabara za sayansi katika shule za sekondari, pamoja na kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi. Kiasi cha Shilingi milioni 824 zimetumika katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kati ya Shilingi bilioni 2.5 zilizopangwa kutumika katika awamu mbili.

Mhandisi Hindi alieleza kuwa utekelezaji wa mradi kwa ujumla ni wa kuridhisha, lakini alitaja maeneo machache yanayohitaji kuboreshwa ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Raslimali na Usimamizi wa Miradi wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, aliihakikishia UNICEF kuwa miradi hiyo itatekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa, na timu ya TEA iko tayari kufanyia kazi mapendekezo ya maboresho yaliyotolewa na UNICEF.