Published at: Wed, Jun 4, 2025 12:18 PM
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeendelea kutekeleza jukumu lake muhimu la kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini. Kupitia miradi mbalimbali, TEA inalenga kuhakikisha kuwa mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji ni bora na salama, ili kutoa nafasi kwa kila mtoto wa Kitanzania kupata elimu bora kwa usawa na bila vikwazo.
Katika muktadha huo, Mamlaka imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu inapatikana kwenye shule za umma. Hii inajumuisha ujenzi wa madarasa, mabweni, matundu ya vyoo, maabara za sayansi, nyumba za walimu, majengo ya utawala na mabwalo ya chakula, ambayo ni mihimili muhimu katika kukuza elimu bora na endelevu kwa watoto wote nchini.
Moja ya miradi muhimu iliyotekelezwa ni ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Ukenyenge, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Mradi huu umetumia takribani shilingi milioni 118, na umefanikiwa kutoa mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na utendaji wa shule, hivyo kusaidia kuboresha zaidi mazingira ya kujifunzia na kufundishia.