The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

TEA yakamilisha ujenzi wa matundu 24 ya vyoo Shule ya Msingi Likunja - Ruangwa

Published at: Wed, Oct 1, 2025 2:29 PM

TEA yakamilisha ujenzi wa matundu 24 ya vyoo Shule ya Msingi Likunja, Ruangwa
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imekamilisha ujenzi wa matundu 24 ya vyoo katika Shule ya Msingi Likunja, wilayani Ruangwa – Lindi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji nchini.
Shule hiyo yenye wanafunzi takribani 470 awali ilikabiliwa na upungufu wa vyoo, hali iliyohatarisha afya na kuathiri mahudhurio ya wanafunzi.
Ujenzi wa vyoo hivyo umezingatia mahitaji ya jinsia zote, kwa kutenganisha matundu ya wavulana na wasichana ili kutoa hifadhi na faragha stahiki, hasa kwa watoto wa kike.
Mradi huu umefadhiliwa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA.
Akizungumza wakati wa makabidhiano mwezi Aprili 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, alisema mradi huu ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwenye mazingira bora, rafiki na salama.
Uongozi wa shule na jamii uliipongeza TEA kwa ufadhili huo na kuahidi kushirikiana katika utunzaji wa vyoo hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu.