The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

TEA yatumia Mil 750 kujenga shule ya mchepuo wa kiingereza ya Msangaalee- Dodoma

Published at: Thu, Dec 7, 2023 4:25 PM

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa inaousimamia imetumia Sh. Milioni 750 kufadhili ujenzi wa Shule ya Msingi Msangalalee  ya  Mtaala wa Kiingereza  ambayo  imeanza rasmi muhula wa masomo Januari 2023 kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo leo tarehe 18 Aprili, 2023, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Dina Mndesha amesema shule hiyo ya umma kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 215 ikiwa na walimu 16.


‘Naishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu kwani shule hii ya mchepuo wa kiingereza imekuwa shule ya umma ya mfano kutokana na ubora wa miundombinu yake katika jiji la Dodoma, amesema Mndesha Mwalimu Mkuu wa shule hiyo”
Ameongeza kuwa kumekuwa na idadi kubwa ya maombi ya udahili na kwamba wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo wanatoka sehemu mbali mbali za jiji la Dodoma.


Kuhusu mikakati ya kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri, Mwalimu Mndesha amesema, wamejiwekea utaratibu wa kuwatambua na kuwapa motisha walimu ambao  wanafunzi wao wanafanya vizuri katika mitihani ya kila mwezi.


Aidha, uongozi wa shule unafanya kazi kwa karibu na wazazi wa wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi wanazingatia masomo, pale tunapoona mwanafunzi analega katika masomo tunawasiliana na mzazi ili kupata suluhu.

Mfuko wa Elimu wa Taifa umetoa ufadhili wa Sh. milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo  itakayotoa elimu kwa lugha ya kiingereza katika mwaka wa fedha wa 2021/ 2022 kwa lengo la kusaidia jitihada za Serikali za  kutoa elimu bora. Ujenzi huo umejumuisha jengo la utawala, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.