The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

UFADHILI WA TEA KATIKA UJENZI WA MABWENI WACHANGIA UFAULU WA WANAFUNZI

Published at: Thu, Dec 7, 2023 3:41 PM

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa leo tarehe 27 Septemba, 2022 amefungua rasmi mabweni mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari ya Kainam ya Mbulu Mkoani  Manyara.

Akifungua mabweni hayo, Mhe. Bashungwa ameipongeza TEA kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni hayo.

Mhe Bashungwa amewakumbusha wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa ndio jukumu lao la msinigi na  kuongeza kuwa  Serikali  imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunza  na kufundishia  hivyo wanafunzi wanapaswa kujifunza kwa bidii.

Awali akizungumza kuhusu mradi huo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kainam, Bw. Atnasi Massay amesema mradi huo umesaidia wanafunzi kufanya vizuri kwani umewaepusha na vishawishi kwa kuishi katika mazingira ya utulivu.

“Kupitia mradi huu wa mabweni watoto wetu wamepata fursa ya kusoma na kupata utulivu  na taaluma ya shule yetu imekuwa kwa maana sasa ni ya kwanza katika Halmshauri ya Mji wa Mbulu kitaaluma kwa matokeo ya  mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne na cha pili mwaka  2020 na 2021” anasema mwalimu huyo ambaye ameipongeza Serikali kwa kufadhili miradi hiyo.

Kwa upande wake Meneja Miradi wa TEA, Masozi Nyirenda amesema TEA kupitia  Mfuko wa Elimu wa Taifa  imetumia kiasi cha Sh. Bilioni 1.39 katika miradi mbali mbali katika mkoa wa Manyara katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016- 2019-2020.