The United Republic of Tanzania

Tanzania Education Authority

Managing The Education Fund

Watumishi wa TEA watakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo.

Published at: Sat, Oct 26, 2024 3:09 PM

Watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wameshauriwa kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni, na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora, uwajibikaji, na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya elimu. 
 
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Erasmus Kipesha katika kikao na watumishi wa mamlaka hiyo kilichofanyika Ijumaa Oktoba 25, 2024 Jijini Dodoma. 
 
Akizungumza na watumishi hao Dkt. Kipesha amesema, TEA inasimamia uboreshaji miundombinu ya elimu pamoja na utafutaji rasilimali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu hivyo ni lazima kila mtumishi afanye kazi kwa bidii, weledi na maadili ili kufikia malengo.
 
Aidha Dkt. Kipesha amesisitiza kwamba, moja ya eneo linalohitaji weledi na uadilifu ni utunzaji wa vifaa vya ofisi pamoja na matumizi sahihi ya vifaa hivyo kama yalivyoanishwa. 
 
Eneo lingine alilolitaja ni matumizi ya mifumo mbalimbali ya Serikali ambayo inamtaka kila mtumishi kuitumia kila siku katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria. 
 
Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka na kushauri sehemu za kuboresha ili kuongeza ufanisi zaidi na kuisaidia mamlaka kufikia malengo iliyojiwekea.